Mwanza kuandaa bonanza la Umisseta Aprili 29

MWANZA imeandaa bonanza la uzinduzi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).

Akizungumzia kuhusu bonanza hilo, Ofisa Michezo wa Manispaa ya Ilemela, Kizito Bahati alisema litafanyika Aprili 29 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

“Mwaka huu mashindano ya Umisseta yatafanyika mkoani kwetu katika Chuo cha Ualimu Butimba (TTC) na tumefanikiwa kupata mdhamini ambaye ni Coca Cola, mdhamini wetu atafanya uzinduzi huu pamoja na wasimamizi (Ofisa michezo) na walimu wa michezo,” alisema Kizito.

Kizito alithibitisha kuwa michezo itakayokuwepo ni soka na mpira wa kikapu kwa wavulana na wasichana na washiriki watatoka katika shule za sekondari kutoka wilaya za Nyamagana na Ilemela.

Bonanza hilo la uzinduzi la umisseta litaanza saa mbili kamili na kuisha saa saba mchana na mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela.

“Mashindano ya Umisseta yameanza kwa ngazi za awali, mashuleni ila mashindano ya mkoa yatafanyika Juni Mosi,” alisema.

Kwa mujibu wa Kizito Mwanza utatoa washiriki wa Umisseta katika michezo ya soka, netiboli, kikapu, wavu, mpira wa mikono, soka kwa wenye ulemavu wa kutosikia, Golball kwa wenye ulemavu wa macho.